Deuteronomy 16

Pasaka

(Kutoka 12:1-20)

1 aShikeni mwezi wa Abibu, na kuiadhimisha Pasaka ya Bwana Mwenyezi Mungu wenu, kwa sababu katika mwezi wa Abibu, Mungu aliwatoa Misri usiku. 2 bMtatoa dhabihu ya Pasaka ya mnyama kwa Bwana Mwenyezi Mungu wenu kutoka kundi lenu la mbuzi na kondoo au la ng’ombe, mahali pale ambapo Bwana atapachagua kama makao kwa ajili ya Jina lake. 3 cMsile nyama hiyo pamoja na mikate iliyotiwa chachu, lakini kwa siku saba mtakula mikate isiyotiwa chachu, mikate ya kujitesa, kwa sababu mliondoka Misri kwa haraka, ili kwamba siku zote za maisha yenu mpate kukumbuka wakati wenu wa kuondoka Misri. 4 dChachu isionekane katika mali zenu katika nchi yenu yote kwa siku saba. Nyama yoyote ya dhabihu mtakayotoa jioni ya siku ya kwanza isibakizwe mpaka asubuhi.

5Kamwe msitoe dhabihu ya Pasaka katika mji wowote ambao Bwana Mwenyezi Mungu wenu amewapa, 6 eisipokuwa mahali atakapopachagua kama makao kwa ajili ya Jina lake. Hapo ndipo lazima mtoe dhabihu ya Pasaka jioni, jua litakapotua, iwe kumbukumbu yenu ya kutoka Misri. 7 fOkeni na mle mahali pale ambapo Bwana Mwenyezi Mungu wenu atakapopachagua, kisha asubuhi mrudi kwenye mahema yenu. 8 gKwa siku sita mtakula mikate isiyotiwa chachu na siku ya saba fanyeni kusanyiko kwa ajili ya Bwana Mwenyezi Mungu wenu na msifanye kazi.

Sikukuu Ya Mavuno

(Kutoka 34:22; Walawi 23:15-21)

9 hMhesabu majuma saba tangu wakati mnapoanza kuchukua mundu kuvuna nafaka. 10 iKisha msherehekee Sikukuu ya Majuma kwa Bwana Mwenyezi Mungu wenu kwa kutoa sadaka ya hiari kwa kadiri ya baraka ambayo Bwana Mwenyezi Mungu wenu amewapa. 11 jShangilieni mbele za Bwana Mwenyezi Mungu wenu mahali atakapopachagua kama makao ya Jina lake, ninyi, wana wenu na binti zenu, watumishi wenu wa kiume na wa kike, Walawi walio katika miji yenu, na wageni, yatima na wajane waishio miongoni mwenu. 12 kKumbukeni kwamba mlikuwa watumwa kule Misri na mfuate amri hizi kwa uangalifu.

Sikukuu Ya Vibanda

(Walawi 23:33-43)

13 l mAdhimisheni sikukuu ya vibanda kwa siku saba baada ya kukusanya mazao yenu ya nafaka na kukamua zabibu. 14 nMfurahie sikukuu yenu, ninyi, wana wenu, binti zenu, watumishi wenu wa kiume na wa kike, Walawi, wageni, yatima na wajane ambao wanaishi katika miji yenu. 15 oKwa siku saba mtaiadhimisha sikukuu ya Bwana Mwenyezi Mungu wenu katika mahali atakapopachagua Bwana. Kwa kuwa Bwana Mwenyezi Mungu wenu atawabariki katika mavuno yenu na katika kazi zote za mikono yenu na furaha yenu itakamilika.

16 pWanaume wenu wote lazima wajitokeze mara tatu kwa mwaka mbele za Bwana Mwenyezi Mungu wenu mahali atakapopachagua: kwa ajili ya Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu, Sikukuu ya Majuma, na Sikukuu ya Vibanda. Hakuna mtu atakayejitokeza mbele za Bwana mikono mitupu: 17 qKila mmoja wenu ni lazima alete zawadi kulingana na jinsi ambavyo Bwana Mwenyezi Mungu wenu alivyowabariki.

Waamuzi

18 rWateue waamuzi na maafisa kwa kila kabila lenu katika kila mji ambao Bwana Mwenyezi Mungu wenu anawapa, nao watawaamua watu kwa usawa. 19 sMsipotoshe haki wala msifanye upendeleo. Msikubali rushwa kwa sababu rushwa hupofusha macho ya wenye busara na kugeuza maneno ya wenye haki. 20 tMfuate haki na haki peke yake, ili mweze kuishi na kuimiliki nchi ambayo Bwana Mwenyezi Mungu wenu anawapa.

Kuabudu Miungu Mingine

21 uMsisimamishe nguzo yoyote ya Ashera kando ya madhabahu mliyomjengea Bwana Mwenyezi Mungu wenu, 22 vwala msisimamishe jiwe la kuabudu, kwa maana Bwana Mwenyezi Mungu wenu anavichukia vitu hivi.
Copyright information for SwhKC